Mheshimiwa Koigi Wa Wamwere
Jana Kenya ilimpoteza Waweru Mburu, mmoja wa Mashujaa wake katika uanahabari wa radio.
Kwa njia ndogo, Waweru Mburu alifanya kazi na nyumba ya habari ya Royal Media au Citizen kama msimamizi wa idhaa ya Kiswahili. Kwa njia kubwa lakini, Waweru alifanyia Kenya nzima kazi kama mchambuzi wa habari na mwalimu wa umma.
Waweru alipendwa sana na wasikilizaji na mashabiki wa kipindi chake cha “Yaliyotendeka”. Hata hivyo wasiopenda ukweli na haki walimchukia sana.
Kwa jumla, watu tofauti watamkumbuka Waweru Mburu kwa namna na mambo mengi tofauti lakini hiba yake kuu itakuwa ni ya ujasiri wake wa kipekee. Waweru hakuogopa kusema ukweli hata kama ulikuwa mchungu kwa wenye uwezo wa kila aina. Katika makala yake Waweru Mburu hakuogopa kusema ukweli hata kama ukweli huo ulimchukiza nani au nani. Wakati mwingine Waweru Mburu aliikosoa serikali na wakati mwingine akaukosoa upinzani.
Lakini kusema ukweli hasa kwa niaba ya walalahoi na wanyonge kulihitaji ujasiri wa kipekee kwani kunasheheni hatari nyingi kubwa.
Waweru Mburu alikuwa fahari mtaifa ambae hangekaa katika zizi moja na ukabila.
Lakini katika kupigana na ukabila Waweru Mburu alikuwa mzalendo mkubwa aliyeweka maslahi ya taifa juu ya usalama wake binafsi.
Ijapoluwa kuna waliomwita Waweru Mburu msaliti au adui wa makabila yao kwa kupinga ukabila, naamini Waweru Mburu, kwa kupinga ukabila na ubwanyenye, alinunua passipoti yake ya kwenda Mbinguni na hivi sasa yuko na Mungu wake.
Na ijapokuwa haya yatasemwa na Kanisa wakati wa mazishi yake, lakini maishani yake mafupi, Waweru Mburu alipigana vita vyema, mwendo aliumaliza na imani aliiweka na kwa hivyo Mungu amempokea kwake.
Hatimaye tusisahau Waweru Mburu hakufa kwa ukongwe na angeishi miaka mingine mingi kama sio kuuawa na Saratani ile ile inayowaua Wakenya kwa maelfu kila mwaka.
Kama tungalikuwa tumejiendeleza zaidi kiuchumi na kihospitali, labda Waweru na Wakenya wengine wengi bado wangalikuwa na sisi baada ya kuushinda ugonjwa badala ya kuuawa nao.
Itakuwa basi ni heshima yetu kwa Waweru Mburu, kama tunapomkumbuka, tutajikusudisha na kujitolea zaidi kuboresha huduma zetu za afya ili watu wetu wanaokufa kwa ugonjwa na mahitaji mengine mengi ya lazima kama kukosa chakula, waishi maisha marefu zaidi.
Ivyo hivyo, serikali imheshimu Waweru Mburu, sio tu kwa kumpa mazishi ya kitaifa, lakini pia kwa kuweka bidii za kumaliza mgomo wa makaktari unaoendelea sasa katika kaunti ya Nakuru.
Waweru Mburu, Mungu akuweke mahali pema peponi na achukue pahali pako kama mlinzi wa familia na nyumba yako hapa duniani.
Mungu hamsahau mja wake mwema. Inshallah.
Leave a Reply